Monday , 16th Mar , 2015

Klabu ya Yanga imesema mechi za Ligi kuu zinazoendelea zimekuwa kama sehemu ya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya FC Platinum ya nchini Zimbabwe.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkurugenzi wa kitengo cha Habari na mawasiliano cha Klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema, baada ya kumaliza mechi ya jana ambayo waliweza kupata ushindi wa goli 5-1 zinaisaidia timu Jumatano watakuwa na mechi dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Muro amesema, baada ya Mechi na Kagera, siku ya Jumamosi watasafiri kuelekea jijini Tanga kucheza na Mgambo na baada ya hapo watarejea jijini Dar es salaam kumalizia mechi yao ya kiporo dhidi ya JKT Ruvu na baada ya hapo kikosi hicho kitaelekea nchini Zimbabwe kwa ajili ya kumalizia ungwe ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho.

Muro amesema, kwa upande wa Timu ya FC Platinum ni nzuri ila ushirikiano wa wachezaji na wawapo uwanjani umeweza kusaidi timu hiyo kuweza kufanya vizuri na kusonga mbele zaidi.