Wenyeji Toto ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kuptia kwa Kimanzi kunako dakika ya 39, bao hilo likidumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
Mabao ya Yanga yamepatikana katika kipindi cha pili kupitia kwa Amis Tambwe mwanzoni mwa kipindi cha pili, na beki Juma Abdul dakika ya 79 baada ya kutokea piga nikupiga langoni mwa Toto na Juma Abdul kukutana na mpira uliokuwa umeokolewa, ambapo aliachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.
Kwa matokeo haya, Yanga imezidi kufukuzia ubingwa wake kwa kufikisha point 65, huku ikiwa na mechi 4 mkononi.
Wapinzani wa Yanga ambao ni Simba na Azam wanakutana kesho katika dimba la Taifa, ambapo azam ndiyo inashika nafasi ya pili na point 58, huku Simba ikiwa na point 57.
Katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga, African Sports imewaadhibu wapinzani wao wa jadi Coastal Union kwa bao 1-0.
African Sports imecheza ikiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 60 baada ya mchezaji wake mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 30.
Kwa matokeo haya African Sports imefikisha point 26, na inahitaji kushinda mechi mbili zilizobaki ili iweze kujinasua katika shimo la kushuka daraja.
Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar imeichapa Mbeya City bao 1-0 katika dimba la Manungu Morogoro, Mwadui imeifunga Stand United mabao 2-1 na jijini Mbeya Prisons imelazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Ruvu.