
Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Dawa za kulevya inaunga mkono lengo la Serikali kuandaa sheria maalum itakayoipa mamlaka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa na maamuzi ya mwisho dhidi ya taasisi nyingine kama TBS na TFDA.
Akiongea wakati wa kutoa maazimio ya kamati hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo Hasna Mwilima amesema kwa hali iliyopo sasa inatishia uhai wa ofisi ya Mkemia Mkuu kwa kutokuwa na mipaka ya kimajukumu kati ya mashirika mengine ya viwango na ofisi hiyo ambayo inaonekana haiendeshwi kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa serikali Pofesa Samweli Manyere amesema kuwa tatizo la kuingiliwa kimajukumu ni kubwa na kutoa mfano ambapo amesema Jeshi la Polisi linajiandaa kufungua maabara yake itakayowawezesha kupima kesi zao wenyewe, hali hiyo ni mbaya kwani itafika mahali kila shirika litaanzisha maabara yake na kuidhoofisha Ofisi ya Mkemia Mkuu kimajukumu.
Aidha kamati pia imepitisha maazimio ya kuwapima vijana waliopo mashuleni kama wanatumia dawa za kulevya au laa kwa lengo la kujua mapema athari walizopata na jinsi ya kuweza kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizo.