Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Mustafa Selebosi
Madiwani hao pia wamekiri kumaliza tofauti iliyokuwepo sanjari na kufanya uchaguzi wa kuunda kamati za Halmashauri hiyo.
Kikao cha leo ni muendelezo wa kikao cha tarehe 19 Desemba mwaka jana ambapo vurugu zilianza baada ya Mkurugenzi wa jiji kutangaza nafasi ya umeya kuchukuliwa na Chama cha Mapinduzi CCM ambapo Chama cha Wananchi CUF hakikuridhika na matokeo hayo.
Akifungua kikao cha kwanza cha baraza la madiwani Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Mustafa Selebosi amesema wameamua kuondoa tofauti zao na kuungana kwa pamoja ili waweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua sambamba na kufanya kazi za Halmashauri kwa pamoja ili kuliletea Jiji la Tanga maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Tanga Daudi Mayeji aliwashukuru madiwani hao kwa kuamua kwa moyo mmoja kufanya kazi ya kuungana kwa pamoja ili waweze kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua katika maeneo yao.
Mayeji alisema kwa muda mrefu swala hilo limekuwa likiwapa wakati mgumu kutokana na vikao vya baraza kutokaliwa na kueleza kuwa viongozi wa serikali na vyama wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kuwaunganisha madiwani hao sanjari na kumaliza tofauti hiyo.
Naye Mbunge wa jiji la Tanga kupitia Chama cha Wananchi CUF Mussa Mbaruku amesema madiwani ni jicho la Serikali katika Halmashauri hivyo wanapaswa kutambua wajibu wao ili penye hitilafu warekebishane na kuwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa nafasi aliyonayo ili Halmashauri iweze kupiga hatua.