Tuesday , 14th Aug , 2018

Rapa Moni Centrozone amefunguka na kukanusha taarifa za yeye kukataa kuwasaidia 'kuwavimbia' wasanii wenzake hasa wanaotoka jiji la Dodoma katika kuwasaidia kazi zao za sanaa na kudai watu hao wanaotoa malalamiko hayo ni wavivu hawataki kujishughulisha.

Rapa Moni Centrozone

Moni ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio kila siku ya wiki kuanzia majira ya saa 7:00 mchana hadi 10:00 jioni, baada ya kuwepo tetesi mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuwa msanii huyo hapendi kuwasaidia wenzake.

"Malamiko mengi huwa nakutana nayo kwenye magroup ya Dodoma na mengine yaliyokuwepo na mara nyingi hao ambao wanalalamika ni wavivu hawataki kufanya kazi. Ila wapo baadhi ya wasanii ambao wanajua mchango wangu kwao na wala hawatoi malalamiko yoyote zaidi ya kutoa kazi zao", amesema Moni.

Kwa upande mwingine, Moni Centrozone amedai yeye ni miongoni wa watu walioweza kuisaidia kwa namna moja ama nyingine kundi la ROSTAM ambalo lina muunganiko na wasanii wawili wa kurapu ambao ni Roma Mkatoliki pamoja na Stamina, licha ya kuwa haongei na watu hao kwa sasa.

Moni Centrozone amekuwa ni mtu mwenye mtazamo tofauti mara nyingi hasa pale anapokuwa anaulizwa swali linalokuwa lina muhusu rapa Roma Mkatoliki.

Mgogoro wa Moni na Roma unadaiwa kusababishwa na Roma kutoa wimbo uliokuwa unazungumzia tukio lao la kutekwa mwaka mmoja uliopita kutokea sasa, ambapo Roma alizunguzia tukio hilo kwenye wimbo pasipo kumuhusiasha mtu yoyote jambo ambalo lilimchukiza Moni na kuona alijichukulia yeye kama kinara mkuu.