Monday , 26th Nov , 2018

Kesi ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe dhidi ya Jamhuri ya ambayo anayeshtakiwa kwa makosa matatu likiwemo la uchochezi na kutoa taarifa za uongo kuhusu mauaji ya polisi na raia wilayani Uvinza mkoani Kigoma inatarajiwa kusikilziwa leo Jumatatu Novemba 26.

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe

Kesi hiyo  ya jinai namba 367 ya mwaka 2018 inayomkabili kiongozi huyo wa chama cha ACT-wazalendo, inatarajiwa kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu aliwataka wananchi wa kawaida na wafuasi wa chama hicho kujitokeza mahakamani kufuatilia kesi ya kiongozi huyo.

Oktoba 30, 2018, Kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kuwa tuhuma alizotoa Zitto hazina ukweli wowote dhidi ya mauaji hayo hakuna watu 100 waliouawa na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

Hakuna watu mia moja waliouawa. Tunamtaka Zitto aonyeshe vielelezo vya hayo anayosema au aje atuonyeshe makaburi ya watu hao anaosema wameuawa Kigoma”, alisema Kamanda Ottieno