Tuesday , 27th Nov , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amempongeza Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa kwa kitendo cha kuhudhuria kuungana na serikali katika miradi ya maendeleo.

Pichani kulia, mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe akiwa na Edward Lowassa, kushoto Rais Dkt. Magufuli na Lowassa wakiwa Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli amefunguka hayo wakati akihutubia katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambapo amesema kuwa pamoja na kumshinda katika uchaguzi mkuu wa 2015 lakini bado hakuwa na kinyongo nae na kukaa kimya huku wasiohusika wakipiga kelele.

"Maendeleo hayana chama, ndio maana leo Mzee Lowassa yupo hapa, nikushukuru kwa utulivu wako nilipokutupa chini baada ya uchaguzi ulikaa kimya, maana tuligombea mimi na wewe lakini wengine wanapiga kelele tu, kwakweli nikupongeze kwa uzalendo", amesema Rais Dkt. Magufuli.

Aidha ameongeza kuwa, "Naomba mzee Lowassa ukatusaidie kuwaelekeza na wenzako unaowaongoza huko namna ya uzalendo vinginevyo wataishia magaerezani ili wakajifunze namna ya kuziheshimu sheria za Watanzania".

Katika hatua nyingine Rais Dkt. Magufuli amempongeza pia Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuanzisha wazo hilo la kujenga maktaba na yeye kuwa sehemu ya utekelezaji.

"Napenda niipongeze serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu mzee Kikwete, kwakuwa yeye ndio aliyeandaa wazo hili mimi nmeendeleza tu, kuweka kwangu jiwe la msingi na leo kuzindua haimaanishi kuwa mimi ndiye nimefanikisha hili", amesema Magufuli.