
Lazaro Nyalandu.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, mbunge huyo wa zamani wa Singida Kaskazini ameandika, “Jumapili ya leo tuungane sote kumwombea mwenyekiti Mbowe, Matiko na wote waliowekwa kizuizini popote Tanzania.”
“Kwa sababu moja, au nyingine imeandikwa haki huinua Taifa. Wenye Mamlaka wakaone fahari kutenda haki bila kukawia zaidi. Kama Taifa, tusimame pamoja nao.”
Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, anayesikiliza kesi hiyo Novemba 23, 2018 kutokana na maombi ya upande wa mashtaka yaliyodai wameshindwa kuhudhuria mahakamani bila sababu za msingi katika kesi yao iliyopangwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Viongozi hao wamekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam chini ya hati ya dharura wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.
Novemba 30, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisimamisha usikilizwaji wa rufaa ya Mbowe na Matiko hadi rufaa ya serikali itakapoamuliwa na Mahakama ya Rufani.
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Sam Rumanyika unamaanisha kwamba, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Matiko ambaye ni mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) wataendelea kusota gerezani kwa siku zisizojulikana wakisubiri Mahakama ya Rufaa kupanga siku ya kusikiliza rufaa hiyo.