Saturday , 22nd Dec , 2018

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku vigodoro na disko toto katika sikukuu ya Krisimasi kwa kuwa vitendo vinavyofanyika katika shughuli hizo ni kinyume na utamaduni wa Watanzania.

Pichani, watu wakicheza muziki.

Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 22, 2018 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa, ambapo ameeleza jinsi polisi walivyojipanga kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, huku akitahadharisha vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwataka wananchi kusherehekea kwa amani na utulivu.

"Doria zitaimarishwa kwenye maeneo yote zikiwemo nyumba za ibada, fukwe, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu", amesema Mambosasa.

Ameongeza, "Disko toto ni marufuku Kanda Maalumu ya Dar es salaam. Watu washerekee na watoto wao kwenye maeneo ambayo ni salama ili sikukuu hii isije ikatuletea misiba isiyo ya lazima”.