Tuesday , 3rd Sep , 2019

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi kwa kumteua Prof. Fredrick Cassian Kahimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO).

Rais Magufuli

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Kahimba umeanza tarehe 31 Agosti, 2019, ambapo kabla ya uteuzi huo, Prof. Kahimba alikuwa Profesa Mshiriki na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utawala na Fedha), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine SUA ni miongoni mwa vyuo vikuu hapa nchini vilivyotoa wahadhiri wengi zaidi katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye serikali ya Rais Magufuli tangu aingie madarakani, ambapo ndani ya miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2019, jumla ya wahadhiri watano wameteuliwa.

Mnamo Machi 26, 2016, Rais Magufuli alimteua Prof. Siza D. Tumbo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), nafasi ambayo iliachwa wazi na Evarist Ng'wandu.

Mei 30, 2016, Rais Magufuli alimteua Prof. Apollinaria Elikana Pereka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (Dar es salaam Institute of Technology - DIT) kabla ya kumteua Prof. Sylvester Michael Mpanduji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) mnamo 18 Julai 2016.

Oktoba 26, 2018, Rais Magufuli alimteua Prof. Joyce L.D Kinabo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (Tanzania Food and Nutrition Centre -TFNC). Prof. Kinabo alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Idara ya Sayansi na Teknolojia ya Chakula.