Tuesday , 3rd Sep , 2019

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, amesema Bunge hilo lina mpango wa kuacha kutumia mfumo wa sasa wa makaratasi Bungeni, kwa ajili ya kuwapa Wabunge nyaraka mbalimbali, watakachofanya sasa ni kuhamia katika mfumo wa Digitali, kwa kuwawekea kupitia kwenye simu zao.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma leo, wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 16, wa Bunge la 11, ambapo amesema katika Afrika Mashariki, Tanzania pekee ndiyo nchi ambayo Bunge lake bado linatumia karatasi.

Spika Ndugai amesema kuwa "sisi ndiyo Bunge pekee Afrika Mashariki ambao tunaendekeza Makaratasi mengi, wenzetu hawatumii, tunaanza na hii 'Order Paper' halafu tutaenda kidogo kidogo"

"Mpaka tufike hatua dawati la Mbunge liwe safi, naombeni mhakiki simu zenu na barua pepe, tunaanza kuwapatia nyaraka." ameongeza Spika Ndugai.

Leo Septemba 03, 2019 mkutano wa Bunge la 16 umeanza jijini Dodoma, ambapo Miraji Mtaturu aliapishwa kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, akirithi nafasi ya Tundu Lissu.