
Kutoka kushoto ni January Makamba, Rais Magufuli na William Ngeleja.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa suala la kusamehe ni jambo kuu na la msingi na kusema kuwa ameamua kuwasamehe hao, kwakuwa aliwaona wameomba msamaha kwa dhati ya mioyo yao ukizingatia na yeye humuomba msamaha Mungu aliyemuumba.
''Mimi nakumbuka hivi karibuni kunawatu fulani walinitukana tukana wee, nikakaa nikaprove kuwa sauti ni zao kwa asilimia mia moja, nikawa nakaa nafikiriaa nikasema hawa wakipelekwa kwenye kamati Kuu ya Siasa ya Chama, adhabu itakuwa ni kubwa, nikasema bora ninyamaze lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha nikasema nisipowasamehe nitabaki na majeraha makubwa moyoni mwangu, ambao ni Mheshimiwa January Makamba na William Ngeleja na niliwasamehe na kasahau'' amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameyabainisha hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa wakandarasi, ambapo amewabainishia changamoto zilizopo kwa upande wao, ikiwa ni pamoja na kuendekeza vitendo vya rushwa na kutokuwa na uthubutu wa kuomba tenda pindi zabuni zinapotolewa.
''MiongonI mwa changamoto hizo ni kutokuwa na umoja na ushirikiano miongoni mwa wakandarasi wa ndani inayopelekea mshindwe kupewa miradi mikubwa na kuendeleza vitendo vya rushwa ili mpate zabuni, mwaka jana nakumbuka tulitangaza mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Chamwino kwenda Mjini nilitegemea kabisa Km 20, zitaombwa na wakandarasi wazalendo wala hamkuomba, sasa hapo unaweza kujiuliza wakandarasi wazawa wa makampuni ya ndani hawajui kuomba kazi'' amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi pamoja na Bodi ya wakandarasi, kuhakikisha wanazitafakari kwa kina changamoto zilizopo, ikiwemo kuzidisha ukali kwa wataalamu wanaoenda kinyume na maaagizo, ikiwemo kuhakikisha wanawafutia usajili wakandarasi wasiokuwa waadilifu.