Wednesday , 4th Dec , 2019

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally, amesema Mshauri Mkuu wa ACT - Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, kuna kauli ambazo amezieleza hazikutokea kwenye ziara yake anayoifanya hivi sasa Visiwani Zanzibar, ambapo alidai kumeandaliwa mpango wa kuhakikisha yeye hagombei

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally.

Urais wa Zanzibar kupitia chama chake kipya.

Bashiru Ally ameyasema hayo wakati akizungumza na wanaCCM Mkoa wa Kusini Pemba, alipokuwa akizindua tawi la Ole, jimbo la Ole, ambapo amesema ziara yake ya siku tisa katika Visiwa vya Unguja na Pemba, ina lengo la kuimarisha uhai wa chama na si vinginevyo.

"Maalim Seif hakuwahi kwenye matamko yake ama mikutano yake kunizungumzia kwa ukali na chuki kiasi kile kama alivyofanya, hivyo kama mitambo tu nimeifunga siku tisa mitetemeko hii imeanza kusababisha taharuki, je ikianza kufanya kazi itakuaje, mimi sitaki kumjibu maana kwa bahati mbaya anawashauri wabaya kwa sababu kwa kasi ya ziara yangu asingewezea kufuatilia bila kuwatuma watu, na ziara yangu kote imekuwa hadharani na vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti, nimeshangaa kusikia mambo ambayo hayakutokea kwenye ziara yangu" amesema Katibu Mkuu CCM.

Aidha Bashiru Ally amesema kuwa "katika hili niwaase wanaCCM na Watanzania msimhukumu Maalim Seif kwa kuwa hata yeye anapotoshwa na wanaomshauri, tangu awe mshauri amekuwa hatafuti tena taarifa za kweli, kila anachopokea anakwenda kuropoka".

Hivi karibuni akizungumza na vyombo vya habari Visiwani Zanzibar, Maalim Seif alidai kuna baadhi ya njama zimepangwa ili kumkosesha yeye uhalali wa kugombea Urais kwenye Uchaguzi wa 2020.