
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Ameyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika mikutano iliyofanyika wilaya ya Kati na wilaya ya Kusini alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Kusini Unguja.
“Watanzania tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu, hivyo ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu tusiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani watu hao hawana tija.”
Waziri Mkuu ambaye awali alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari ya Bwejuu, mradi wa kilimo cha kisasa Jozani na kuzindua jengo la mama na mtoto Bambi. Amesema hayo yote ni matunda ya muungano hivyo, hawana budi kuendelea kuudumisha.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari ya Bwejuu, Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa mkandarasi anayejenga maabara hiyo awe amekamilisha kazi hiyo.
Pia, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub Mohammed Mahmoud ahakikishe watumishi wanatenga muda wa siku nne kwa wiki kwa ajili ya kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao hususan ya vijiji.
Vilevile, Waziri Mkuu aliagiza Maafisa kilimo wahamishiwe vijijini ili waweze kuwasimamia vizuri wakulima ikiwa ni pamoja na kuwashauri namna bora ya kulima kwa kufuata kanuni na matumizi mazuri ya pembejeo.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wananchi wote bila ya kujali dini, kabila, rangi wala itikadi za chama kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wananufaika na kuhudumiwa bila ya kubaguliwa kwa namna yoyote.
#HABARI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania washirikiane katika kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar na wasiruhusu watu kuwagawa. pic.twitter.com/VAJNmUFtuP
— East Africa Radio (@earadiofm) January 18, 2020