Monday , 10th Feb , 2020

Kampeni ya NAMTHAMINI inayoendeshwa na East Africa Television na East Africa Radio kwa mwaka wa nne mfululizo, imewafikia wanafunzi zaidi ya elfu moja mkoani Iringa na kuwapatia taulo za kike zitakazowasaidia kwa mwaka mzima kutokosa masomo kwa changamoto ya ukosefu wa pedi wakati wa hedhi

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Lukosi Wilayani Kilolo Iringa wakipokea msaada wa pedi.

Baadhi ya wanafunzi katika shule tofauti tofauti za wilayani Kilolo, wamesema kuwa ukosefu wa taulo hizo za kike imekuwa ni moja ya changamoto inayowafanya baadhi yao hasusani wanaotoka familia duni kushindwa kuhudhuria masomo kikamilifu, wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.

Anifa Athumani ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari Lukosi ambayo ilipokea msaada wa zaidi ya pakiti 3568, amesema sasa tatizo la kukosa masomo limetatuliwa.

Kwa upande wake Shaila Musa, mwanafunzi wa Sekondari Mazombe ambayo imenufaika kwa kupata pakiti 2640 za pedi, amekiri kupitia changamoto ya kukosa masomo wakati wa hedhi hivyo kupitia Namthamini ataweza kusoma kwa mwaka mzima.

Mwakilishi wa East Africa Television na East Africa Radio Deogratius Kithama, akikabidhi msaada wa pedi katika shule ya Sekondari Lukosi wilayani Kilolo mkoani Iringa wiki iliyopita. Pedi hizo zimetokana na Kampeni ya Namthamini inayoendeshwa na vituo hivyo kwa mwaka wa nne mfululizo, ambapo kwa Iringa imezifikia shule tatu za Sekondari ambazo ni Lukosi Sekondari, Mazombe Sekondari na Nyalumbu Sekondari.

Shule nyingine ambayo imepata pedi zaidi ya pakiti 1604, ni Nyalumbu ambapo mwanafunzi Theresia Richard, ameishukuru East Africa Television na East Africa Radio na kuahidi watajituma zaidi ili wafaulu.

Kwa upande wake Antokiye Kivanda ambaye ni mwalimu wa malezi katika shule ya Sekondari Mazombe ameeleza hali ilivyo katika shule hiyo kuwa changamoto ya pedi kwa wasichana ni kubwa hivyo msaada uliotolewa utawasaidia kuongeza mahudhurio kwa wanafunzi.

Aidha akizungumza na timu ya East Africa Television na East Africa Radio ofisini kwake, Afisa Elimu Mkoa wa Iringa Aloyce Kamamba ameeleza kufurahishwa na kampeni hiyo huku akiomba izidi kuongeza idadi ya shule mkoani humo kwa mwaka ujao.