Wednesday , 26th Aug , 2020

Msanii wa Bongfleva Aslay Isihaka amenyoosha maelezo kwa kutaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, kuvichukulia hatua baadhi ya vyombo vya habari vya mitandaoni "Online Media" baada ya kumzushia kwamba amefariki dunia. 

Msanii wa BongoFleva Aslay Isihaka

Kupitia post yake aliyoweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram msanii huyo ameeleza kuwa "Inasikitisha na kushangaza sana unawezaje kumzushia mwanadamu mwenzako kifo na mabaya mengi, wanaofanya hivi ni Watanzania wa kawaida kama sisi ambao tulitamani watupe habari na burudani na wao wapate riziki, lakini wako bize kutupotosha na hata kuharibu majina yetu

"Nawaomba sana TCRA wasiache kuzichukulia hatua online Tv makanjanja wengine wanaopotosha umma, tuna imani nanyi TCRA na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine, watu kama hawa wakiachwa, wanachafua taswira nzuri ya vyombo vingine vinavyofanya kazi kwa weledi, naheshimu sana waandishi wote bila kujali ukubwa wa vyombo vyao, lakini hawa makanjanja wachukuliwe hatua na kutokomezwa kabisa" ameongeza 

EATV & EA Radio Digital imejaribu kumtafuta msanii huyo ili kutolea maelezo zaidi lakini imeshindikana kumpata hewani kwa sababu alikuwa hapatikani.