Monday , 16th Nov , 2020

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango ameahidi kusimamia kikamilifu ubadhirifu wa fedha za umma huku akiwaonya watu wazembe na kuwataka wawapishe mapema .

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Philip Mpango

Akizungumza mara baada ya kuapishwa katika ofisi za Ikulu mkoani Dodoma Dkt.Mpango amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kwa mara nyingine tena kuendelea kuwa Waziri wa Fedha na Mipango huku akiwashukuru watanzania wote.

“Uzembe, wizi na ubadhirifu wa fedha za umma hilo nitalitilia kipaumbele cha juu bado naona shida kwenye miradi ya maendeleo bado tunaibiwa  kuna shida nitasimamia ili tuokoe fedha za hawa wanyonge zifanye kazi yake  na hao wazembe kwa kuwa umenipa kisu watupishe mapema kwa sababu mzigo huu ni mkubwa sana kazi hii ni gunia la misumari kwa hiyo watupishe.” Alisema Dkt. Mpango

Aidha Dkt.Mpango ameongeza kuwa  upo uwezekano katika kipindi kifupi na chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania itakuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati kwa kiwango cha juu.

“Huko niliko kwenda kwa ajili ya kampeni umaskini bado ni mkubwa bado tunahitaji kufanya kazi kwa bidii kuwatumikia watu wetu fursa zipo nyingi na inawezekana kabisa  na ndani ya kipindi kifupi na mimi naamini ukiwa bado kwenye kiti chako tutakuwa  nchi yenye hadhi ya kipato cha kati kwa kiwango cha juu” Alisema Dkt. Mpango