Monday , 7th Dec , 2020

Wadau na viongozi wa serikali mkoani Singida, Wilaya Ikungi wameomba kuangalia uwezekano wa kufuta dhamana kwa watuhumiwa wa kesi za ubakaji na mimba za utotoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi

Ombi hili linakuja kama pendekezo kufuatia kikao walichoketi baadhi ya wadau na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, cha kupeana mrejesho na namna bora ya kukabiliana na matukio ya ukatili wilayani hapo ambayo yamekuwa yakiumiza vichwa viongozi.

Imebainishwa kuwa baadhi ya watu katika jamii wanashindwa kutoa ushirikiano ipasavyo pindi wanaposhuhudia au kuwa na taarifa sahihi za matukio ya ukatili kwa hofu kuwa wahalifu hao kupatiwa dhamana muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye vituo vya polisi na mahakama hivyo kuhatarisha hali yao kiusalama.

Aidha Jeshi la Polisi wilayani humo limewataka viongozi wa ngazi zote za utatuzi kutoruhusu kesi hizo kumalizwa katika ngazi za familia badala yake zifike mahalai sahihi kwa ajili ya utatuzi maalum hii ikiwa ni kupeana mrejesho juu ya nini kinapaswa kufanyika ili kutokomeza matukio hayo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliwataka watendaji wote wilayani hapo kujikita katika kutoa elimu ili kuepukana na matukio hayo.

Matukio ya ukatili yaliyoibuliwa na shirika lisilo la kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) kwa wilaya ya Ikungi pekee mpaka sasa yamefikia idadi ya 104, huku mengi kati ya hayo yakionekana kumalizwa katika ngazi ya familia kwa kuepusha kadhia hiyo.