Tuesday , 5th Jan , 2021

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa mbunge pekee wa jimbo la  Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, aliyeshinda katika uchaguzi mkuu alikula kiapo cha nafasi hiyo kinyume na msimamo wa chama chake.

Kushoto ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kulia ni mbunge pekee wa CHADEMA aliyeshinda Aida Khenani

Kauli hiyo ameitoa jana jioni wakati akizungumza na umma kupitia ukurasa wa Youtube wa chama hicho na kusema kuwa, mbunge huyo pamoja na madiwani wengine zaidi ya 80 walioshinda na kula kiapo, kosa walilolifanya si la jinai bali walienda kinyume na taratibu za chama na msimamo wa chama hicho ambacho kinaamini kuwa uchaguzi haukufanyika.

"Watanzania wenzangu mbunge wetu wa Nkasi Kaskazini na baadhi ya madiwani wameapa na kuingia kwenye vyombo vya kiserikali kinyume na msimamo wa chama, nguzo kuu ya chama chochote cha kisiasa ni nidhamu, bila hivyo chama hugeuzwa kuwa genge la wahuni lisilo na miiko wala mipaka", amesema Mbowe

"Baada ya uchaguzi mkuu tofauti na wabunge wa viti maalum, mbunge wetu wa Nkasi na madiwani kadhaa hawajatenda jinai bali walikaidi ama walikataa kuheshimu msimamo wa chama na chama kitafanyia kazi mazingira ya kila mmoja wao, kitawasikiliza na kuchukua uamuzi stahiki kwa wakati mwafaka zaidi", ameongeza Mbowe.

Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 28, 2020, CHADEMA ilipoteza karibu majimbo yote nchini na kuambulia ushindi kwa mbunge wa jimbo moja la Nkasi Kaskazini.