Wednesday , 3rd Feb , 2021

Klabu ya Manchester United ‘Mashetani wekundu’wamefanya mauaji makubwa kwenye EPL baada ya kupata ushindi wa mabao 9-0 dhidi ya Southampton kwenye dimba la Old Trafford usiku wa kuamkia leo.

(Wachezaji wa Manchester United wakipongezana baada ya Martial kufunga bao.)

Kalamu hiyo ya mabao ilianza baada ya kushuhudia kiungo wa Southampton Alex Jankewitz akioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi Mike Dean baada ya kumkwatua Scott Mc Tominay dakika ya pili ya mchezo na kuifanya timu yake kuwa na mlima mkubwa wa kupanda.

(Mwamuzi wa kati, Mike Dean akimuonesha kadi nyekundu mlinzi wa kati wa SOTON, Jan Bednarek.)

Mlinzi wa kulia wa United, Aaron Wan-Bissaka ndiye aliyefungua ukurasa huo wa mabao, Marcus Rashord akifunga la pili, mlinzi Jan Bednarek aliwapa United bao la tatu baada ya kujifunga na mshambuliaji Edinson Cavani akafunga bao la nne kabla ya kwenda mapumziko.

Baada ya dakika 25 za kipindi cha pili, Anthonio Martial alifunga bao la tano na kuzidi kuwanyongónyesha wapinzani wao na dakika mbili baadaye, kiungo Scott Mc Tominay akafunga bao la sita nje ya 18.

Bao la saba limefungwa na Bruno Fernandes kwa mkwaju wa penalty baada ya Jan Bednarek kumfanyia madhambi Martial yaliyopelekea mwamuzi Mike Dean kumuonesha mlinzi huyo kadi nyekundu ya pili kwa upande wa Southampton katika mchezo huo.

Anthony Martial akafunga bao la nane likiwa la pili kwake katika mchezo huo na alikuwa Daniel James aliyefunga ukurasa huo wa mabao kwa kufunga bao la 9 dakika chache kabla ya mchezo huo kumalizika.

Kipigo hiko kimeweka rekodi ya kuwa kipigo cha pili kikubwa kwa Southampton baada ya kufungwa mabao 9-0 dhidi ya Leicester City October mwaka 2019 kwenye EPL chini ya kocha wake wa sasa Ralph Hassenhult.

Kwa United, si mara ya kwanza kushusha kipigo hicho kikubwa, kwani mwaka 1995 mwezi Machi, Manchester United waliwafunga Ipswitch Town mabao 9-0 na msimu wa mwaka 2011-2012, waliwafunga Arsenal mabao 8-2 kwenye EPL.

Ushindi huo umewafanya Manchester United kufikisha alama 44 sawa na vinara Manchester City, lakini City wakiongoza kwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa licha ya kuwa nyuma kwa micheozo miwili nyuma ya Manchester United.

Southampton wamedondokea nafasi ya 12 wakiwa na alama zao 29 huku kocha wake Hassenhult akiongea kwa uchungu kuonesha kusikitishwa na kipigo hiko ambacho anakipata kwa mara ya pili ndani ya EPL licha ya kuanza ligi vizuri.