Sunday , 21st Feb , 2021

Wanafunzi 180 katika shule ya sekondari ya wasichana Sangiti iliopo kata ya Kirima Kibosho wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamenusurika kifo baada ya mabweni manne ya kidato cha tatu na cha nne ya  shule hiyo kuteketea kwa moto na kuteketeza samani pamoja na mali za wanafunzi.

Pichani mabweni ya Shule ya Sekondari ya Sangiti iliyopo kata ya Kirima Kibosho yakiungua moto.

Akiongea kwa masikitiko Mkuu wa Shule na wanafunzi katika wa sekondari hiyo ya wasichana ya Sangiti wamesema moto huo ulianza majira ya saa 7:50 usiku wakati wanafunzi wakiwa katika sala ya jioni ambapo bado hadi sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana licha ya mali na vifaa vya masomo kuungua moto.

“Moto ulianza kuzuka majira ya saa 7:50 usiku watoto walikuwa ndo wamemaliza kusali na wanajianda kwenda kujisomea mmoja akatoka nje akaona moto akamuita mama matron naye akatoka nje na matron mwingine alikuwa anatokea upande huu wa shuleni akaona moto akapiga kelele na sisi ndo tukapanda na watoto paka sasa hivi hatujajua chanzo ni nini,” alisema Mkuu wa Shule ya wasichana Sangiti, Sista  Julieta Massawe.

Kamati ya usalama ya wilaya ya mkoa wa Kilimanjaro zikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira na Mkuu wa wilaya ya Moshi Alhaji Rajabu Kundya wamesema chanzo cha moto huo hadi sasa hakijajulikana lakini wamebaini vyanzo vingi vya moto katika shule zinatokana na uzembe wa wanafunzi pamoja na usalama mdogo wa mabweni ya shule.

“Hii soketi inayosemekana hapa moto ulianzia ina kama moshi lakini nyaya zake hazionekani kwa hiyo huenda zimeungua kwa moto wa kawaida au moto umeanzia pale wataalamu wa moto watatusaidia, amabacho tumeangalia mpaka sasa kuangalia mazingira ya shule, mahusiano kati ya shule na jamii tunajua kuna mgogoro lakini mkuu wa shule amesema sio lazima iwe sababau kwani mgogoro umeanza tangu siku nyingi na bado hakujawahi kutokea jambo lolote,” alisema RC Anna Mghwira.