Sunday , 14th Mar , 2021

Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Njombe zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya parachichi wakati alipotembelea shamba la Bw. Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe, Machi 12, 2021.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kufuatia umuhimu za zao hilo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie maendeleo ya vikundi vya wakulima wa parachichi na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Waziri Mkuu amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa  kwa  gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujipatia fedha zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama parachichi 

Amesema zao la parachichi limechangia katika kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu wengi wameweza kujiajiri na kuajiriwa, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao hilo kwa kuwa linafaida kubwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amempongeza Bw. Mlimbira kwa kuwa na shamba kubwa la parachichi ambalo limewezesha kutoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuwahamasisha walime zao kwa kuwagawia miche kwa gharama nafuu.