
Mshambuliaji wa Simba, Jose Luis Miquissone 'konde boy'.
Kocha Gomez amesema “Luis amechoka ndio maana tunampumzisha ili aweze kuwa fiti kwa asilimia 100, amekuwa akijitoa kwa ajili ya timu na hilo lipo wazi akishirikiana na wachezaji wenzake ndani ya timu.”
“Ni muhimu kwa wachezaji wote kuweza kupata muda wa kupumzika ili kuwa sawa kwa ajili ya mchezo wetu ambao hautakuwa mwepesi ndani ya dakika 90.”
Maneno ya kocha huyo yanamaanisha kuwa nyota huyo ambayo pia ni kinara wa kutengeneza nafasi za mabao klabuni humo sambamba na Cleotus Chama wote wakitengeneza mabao 9 kwenye VPL, atakuwepo kwenye mchezo huo ila kwasasa yupo kwenye progaramu maalum ya kupumzika ili akusanye nguvu na kuisaidia Simba.
Wekundu wa Msimbazi Simba ambao ni vinara wa kundi A wakiwa na alama 7, watakuwa wenyeji wa Al-Merrick kwenye mchezo utakaochezwa saa 10 jioni kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza bila mashabiki kutokana na taratibu za kujikinga na Covid-19 kutoka CAF.
Kama Simba watafanikiwa kupata ushindi, watafikisha alama 10, hivyo watakuwa wamekanyaga mguu mmoja mbele kwenye kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali licha ya kuwa watakuwa wamesaliwa na michezo miwili, mmoja nyumbani dhidi ya AS Vita na mchezo mwingine dhidi ya Al Ahly ugenini.