Thursday , 18th Mar , 2021

Michuano ya EUROPA ligi itaendelea tena usiku wa leo kwa michezo 8 ya mkondo wa pili hatua ya mtoano ya 16 bora, vigogo AC Milan itacheza dhdi ya  Manchester United saa 5:00 usiku wa leo tarehe 18 Machi 2021 baada ya kutoka sare ya 1-1 Old Trafford kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza.

Wachezaji wa Arsenal wakipongezana baada ya kufunga moja ya bao kwenye mchezo uliopita dhidi ya Olympiacos juma lililopita.

Arsenal wanataraji kucheza dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki saa 2:55 usiku wa leo baada ya Gunners kupata ushindi wa mabao 3-1 wakiwa ugenini kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza.

AC Milani imethibitsha kurejea kwa wachezaji wake nyota, mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic, viungo Hakan Calhanoglu na mlinzi wa kushoto Theo Hernandez waliokosekana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kutokana na majeraha madogo.

Kwa upande wa Manchester United, wamethibitisha kurejea kwa kiungo wake Paul Pogba, kiungo Donny Van De Beek pamoja na mlinda mlango wake David De Gea aliyekosekana kutokana na sababu za kifamilia ilhali washambuliaji Edinson Cavani  na Anthony Martial wamesalia nchini Uingereza.

Nae, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema hakuwa utata wowote kati yake na nahodha wake, Pierre Emerik Aubameyang na nyota wake huyo atakuwa sehemu ya kikosi ambacho kitacheza dhidi ya Olympiacos usiku wa leo huku akisema Bukayo Saka yu hatiani kwani itamlazimu kusubiri majibu ya vipimo vya mwisho.

Arteta ameyasema hayo baada ya kukiri kufanya mazungumzo na mshambuliaji wake huyo tegemezi aliyemuondoa kikosini kwenye mchezo wa ligi kuu England wa watani wa jadi wa kaskazini mwa London, dhidi ya Tottenham Hotspurs ambao Arsenal alipata ushindi wa mabao 2-1.

Michezo mingine itakayochezwa saa 2:55 usiku wa leo ni pamoja na: Dynamo Zagreb ya Croatia dhidi ya Tottenham Hotspurs, Spurs akiongoza kwa mabao 2-0, Molde ya nchini Norway watacheza na Granada ya nchini Hispania, Granada ikiongoza kwa mabao 2-0.

Shakhtar Donestk ya Ukraine itacheza na AS Roma ya Italia, Roma akiwa anaongoza kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza.

Michezo itakayochezwa saa 5:00 usiku wa leo ni: Rangers ya Scotland dhidi ya Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech, uliomalizika kwa sare ya bao moja, Nyambizi wa Hispania, klabu ya Villareal itacheza na Dynamo Kiev ya Ukraine, Villareal akiwa na faida ya mabao 3-0.

Ajax ya Uholanzi itacheza ugenini dhidi ya Young Boys ya Uswizi, huku Ajax akiwa na mabao 3-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza. Droo ya Robo fainali inataraji kupangwa tarehe kesho Ijumaa ya tarehe 19 Machi 2021.