Tuesday , 23rd Mar , 2021

Mlinzi nyota wa timu ya Denver Nuggets na mshambuliaji mahiri wa timu ya Milwaukee Bucks za ligi ya kikapu nchini Marekani, wamechaguliwa kuwa wachezaji bora wa wiki ya 13 kwa kuonesha viwango bora na kusaidia timu zao kufanya vizuri wiki iliyoanzia tarehe 15 hadi 21 Machi 2021.

Picha ikiwaonesha Giannis na Jokic kwenye matukio tofauti tofauti.

Jokic na Giannis wametwaa tuzo hiyo usiku wa kuamkia leo tarehe 23 Machi 2021 huku Jokic akitwaa tuzo hiyo baada ya kucheza michezo minne, akipata ushindi kwenye michezo mitatu na kupoteza mmoja na akiwa na wastani wa kupata alama 26.8, ribaundi 12.3 na wastani wakutengeneza mabao 8.5.

Kiwango hiko kizuri cha nyota huyo raia wa Serbia, kimechangia kuifanya timu yake ya Denver Nuggets kupanda hadi kushika nafasi ya 4 kwenye msimamo wa NBA kwa upande wa Magharibi kwa kushindi jumla ya michezo 25 na kupoteza 17 kati ya michezo 42 waliyocheza msimu huu.

(Giannis (kushoto) akijaribu kumtoka Jokic wakati wawili hao walipokutana msimuu huu kwenye NBA.)

Kwa upande wa Giannis Antetokounmpo, ametwaa tuzo hiyo baada ya kucheza michezo mitatu na kuisaidia timu yake ya Milwaukee Bucks kupata ushindi kwenye michezo yote mitatu na kuwa na wastani wa kupata alama 29.5, ribaundi 12.7 na wastani wa kutengeneza mabao 10. (Tripple double)

Giannis amesaidia kuipandisha Bucks hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa NBA kwa upande wa Mashariki kwa kushinda jumla ya michezo 28, ikipoteza michezo 14 kati ya 42 waliyocheza msimu huu.

Ligi ya kikapu nchini Marekani 'NBA', Inataraji kuendelea tena usiku wa kuamkia kesho kwa michezo sita, mabingwa watetezi wa ligi hiyo timu ya Los Angeles Lakers watakipiga na New Orleans Pelicans saa 8:30 usiku wakati Golden State Warriors watacheza na vinara wa upande wa Mashariki Philadelphia 76ers saa 11:00 Alfajiri ya kuamkia kesho.