Tuesday , 30th Mar , 2021

Aliyekuwa Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango ambaye ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na kusema amepigwa na butwaa na hakuwahi kuota.

Dkt. Philip Mpango

''Namshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu kwa kupendekeza jina langu na kuridhiwa na chama chetu cha CCM kuwa Makamu wa Rais, sikuwahi kuota, nimepigwa na butwaa,'' alisema Dkt. Philip Mpango.

Aidha, Mpango ameongeza kuwa, ''Wakati kipindi cha maswali na majibu kinaendelea sikuwa najua lolote, nilikuwa nahangaika na mishahara ya wabunge ambayo haijalipwa mpaka sasa pamoja na mambo mengine, wala sikujua''.

Uteuzi huyo umekuja kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati. Dk. John Pombe Magufuli na aliyekuwa Makamu wake Mhe. Samia Suluhu Hassan kuapishwa kushika nafasi ya Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kufanya nafasi ya Makamu wa Rais iwe wazi na leo kujazwa rasmi.