Thursday , 22nd Apr , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa wanaotoa taarifa zisizo za kweli mtandaoni juu ya kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa wasilete uchonganishi kwani taarifa ya madaktari iliweka wazi juu ya kifo chake kilikotokana na tatizo la moyo.

Hayati Dkt. John Pombe Magufuli

Rais Mhe. Samia amesema hayo leo bungeni na kuwataka wanaopotosha umma kwa kutoa taarifa kuwa Hayati Magufuli alipewa sumu wawasilishe taarifa zao ili waisikilizwe lasivyo waache kuchonganisha bali wakae na kutafakari juu ya wanachokifanya kama ni sahihi mbele za Mwenyezi Mungu.

“Taarifa tuliyopewa na madaktari juu ya kifo cha Hayati John Magufuli ni kwamba alifariki kutokana na tatizo la moyo lakini kuna watu wanatoa taarifa ambazo si za kweli, kama wana taarifa za maana waje watueleze lakini wasilete uchonganishi. Kuna wanaosema mitandaoni kuwa Hayati Magufuli alipewa sumu, mara fulani walitega kitu, kama wana taarifa za maana waje tuwasikilize,” amesema Rais Mhe. Samia.

Aidha, Rais Mhe. Samia amesema kuwa watawatafuta watu hao wanaosamabaza taarifa zisizo za kweli katika mitandao ya kijamii huku wakiamini kuwa hawatoweza kupatikana.

“Wanaoleta uchonganishi kwenye mitandao nadhani wanafanya hivyo kwa sababu wanajua hatutoweza kuwapata, wanatumia mifumo hiyo huko mingine ambayo bado hatujawa na uwezo wa kuwatafuta, lakini niwaambie tutawatafuta,” amesema Rais Mhe. Samia.