Friday , 23rd Apr , 2021

Mwanazuoni Prof. Issa Shivji ameshauri kuwa kuna umuhimu kwa Serikali kuelekeza ni maeneo yapi yatakuwa yanamanufaa kwa uwekezaji ili wawekezaji wasiwekeze kwenye maeneo yenye manufaa ya muda mfupi.

Prof. Issa Shivji

Prof. Shivji ametoa ushauri huo leo katika mahojiano yake kwenye Kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, wakati akitoa mchango wake kuhusiana na hotuba ya Rais Mh. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni jana.

"Mimi naona kunaumuhimu kwa Serikali kuelekeza maeneo ya uwekezaji ili wawekezaji wasiwekeze kwenye maeneo yenye manufaa ya muda mfupi," amesema Prof. Issa Shivji.  

Kuhusu suala la uwekezaji wa makampuni makubwa Prof. Shivji amesema uwekezaji wa nje hususan katika makampuni makubwa ya kimataifa ni ngumu kudhibiti kwani wanazo njia mbalimbali za kutorosha faida.

Akigusia suala la Shirika la ndege nchini (ATCL) Prof. Shivji ameshauri kuwekeza katika ndege ndogo ndogo kwa ajili ya safari za ndani kutasaidia kulifufua shirika hilo, "Ili kuweza kufufua ATCL ingekuwa rahisi kwetu kuwekeza kwanza kwenye ndege ndogo ndogo kwa ajili ya safari za ndani kabla ya kwenda kwenye ndege za safari za nje," amesema Prof. Issa Shivji.

Aidha, Prof. Shivji ameeleza kuwa ilikujengea tija katika sekta ya kilimo nchini ambayo wazalisha wake wengi wapo vijijni, serikali haina budi kutilia mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji na si kutegemea mvua tu.

"Kunahaja kubwa sana ya kuweka mkazo katika kilimo cha umwagiliaji maji, tusitegemee sana mvua, hili la kilimo cha umwagiliaji maji hatuwezi kutegemea sekta binafsi linahitaji kufanywa na Serikali," amesema Prof. Issa Shivji.