Mmiliki na Kocha wa Mbao Fc ya Mwanza, Ammy Ninje akiwa katika majukumu yake Uwanjani.
Kauli hiyo ya Ninje inafuatia timu yake kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwa madai kwamba waamuzi wamekuwa wakichezesha vibaya mechi zao kiasi cha kupelekea kuwa katika hatari ya kushuka daraja kutoka FDL.
Ninje ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, amesema Ligi Daraja la kwanza ina matatizo mengi ya kiuchezeshaji ambayo yanazinyima haki timu zinazostahili kushinda.
''Sina haja ya kuzungumza sana kwakuwa mimi kwa sasa nipo uwanjani nashuhudia mengi yanayoendelea, nitakutana na wasimamizi wa mpira ili tuone ni mkakati upi utumike ili kuboresha mpira wetu. Tumemsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema inatenga pesa kuiunga mkono Taifa Stars, lakini iwapo hakuna usimamizi mzuri hatutosaidia kitu''Alisema Ninje.
Katika hatua nyingine Ninje ambaye amewekeza zaidi katika soka la vijana amesema hatokata tamaa kuendelea kusimamia mpango wake wa kuwainua vijana ili awapeleke kwenye soka la kimataifa.
Mbao ambayo ilikuwa ni kiboko ya vigogo kwenye soka la Tanzania, iliporomoka daraja msimu uliopita, na sasa ipo kwenye nafasi ya 8 kwenye msimamo wa kundi B lenye timu 10, wakiwa na alama 7 pekee na iwapo haitofanya vyema katika michezo michache iliyosalia itakuwa miongoni mwa timu 4 zitakazoshuka hadi daraja la pili.