Maambukizi ya Ukimwi yapungua kidogo sana 

Wednesday , 12th May , 2021

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko amesema maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yanakadiriwa kufikia watu 68,000 kwa sasa, tofauti na maambukizi ya utafiti uliofanywa mwaka 2016/2017 ambapo maambukizi mapya yalikuwa ni watu 72,000.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko

Akizungumza katika mahojiano yake na Kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, Dkt. Maboko amesema ipo haja ya tafiti kutilia mkazo takwimu za maambukizi mapya ya virusi hivyo ili kujua kama maambukizi yanapungua badala ya kuangalia takwimu za watu wanaoishi na Ukimwi kwani hazitosaidia.

"Maambukizi mapya ya Virusi ya Ukimwi bado yana hati hati japokuwa kuna hali ya kupungua, utafiti tuliofanya 2016/17 kwa mwaka ilkuwa watu 72,000 wamepata maambukizi mapya, sasa hivi kwa makadirio utafiti bado maambukizi mapya ni  watu 68000, kuna dalili za kupungua kwa maambukizi mapya ya Ukimwi ijapokuwa sio kwa kasi tuliyoitarajia," amesema Dkt. Maboko.

Akizungumzia maambukizi kwa upande wa vijana Dkt. Maboko amesema changamoto iliyopo ni kuongezeka kwa kasi ya maambukizi kwa vijana wa miaka 15- 24, huku akieleza kuwa vijana wakike wakiwa na silimia 80% katika maambukizi hayo.

"Changamoto ya maambukizi mapya ni vijana wa miaka 15 - 24 ndio wanaambukizwa zaidi kwa sasa hivi, kwa kila watu 10 wanaoambukizwa virusi 4 wanakuwa ni vijana, ukichukua vijana walioambukizwa 80% ya hao vijana ni wa kike, kwa lugha rahisi kila vijana 10 wanaopata maambukizi mapya 8 ni vijana wa kike na 2 ni wa kiume," amesema Dkt. Maboko.

Pia Dkt. Maboko amesisitiza vijana kuendelea kuchukua tahadhari za kutosha ili kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ili kunusuru kizazi hicho kinachotegemewa na taifa kwa kuwa ni nguvu kazi.