Thursday , 13th May , 2021

Imeelezwa kuwa ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa kundi la vijana hususani watoto wa kike, elimu ya ngono salama haina budi kutolewa kwao ili kupunguza athari za ugonjwa huo.

Vijana wakiwa kwenye mkutano(Picha kutoka mtandaoni)

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Supa Breakfast, Mwanamitindo Mashuhuri nchini Tanzania, Nancy Sumari, amesema kuwa ipo haja ya wazazi kuwa karibu na watoto wao kwani inawajengea kujiamini na kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kupelekea athari mbalimbali ikiwemo kupata maambukizi ya Ukimwi.

"Ili kuepukana na janga la Ukimwi elimu ya ngono salama ni muhimu kwasababu kadri tunavyoendelea linazidi kutuwathiri vijana lazima tuwatahadharishe watoto wetu," amesema Nancy.

Pia mwanamitindo huyo amesema ipo haja ya ajenda iliyotumika miaka ya nyuma ya kulea watoto kama kijiji kurudi upya ili kukilinda kizazi hiki ambacho kipo hatarini.

"Waafrika tuna tamaduni ya kulea watoto kama tupo kwenye kijiji fulani yaani mtoto wakwako ni wa mwenzako, nafikiri hii iliwahi kuwa ajenda yetu kitaifa tuna kila sababu ya kurudi huko tukalinda watoto wetu," amesema Nancy Sumari.

Kwa upande wake mwelimishaji wa vijana kutoka Sitetereki, Victor Mushi ameeleza kuwa  wazazi wanapaswa kuwahusisha vijana wao katika maamuzi wanayoyafanya ambayo yanahusu mustakabali wa maisha yao na kuondoa hofu waliyonayo kwani itasaidia katika kuwaelimisha na kuwasaidia kujikinga zaidi na athari mbalimbali.