Monday , 16th Aug , 2021

Karibu kwenye kuzihesabu zile stori sita kali za kimichezo kupitia’Sports Countdown’ ya ‘Super Breakfast’ kutoka East Africa Radio inayokujia kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa mishale ya saa moja na robo asubuhi . Paul Pogba na Bruno Fernandes wazidi kuwa gumzo EPL.

Gerd Muller aliyefariki dunia sikuu ya jana Agosti 15, 2021 akiwa na umri wa miaka 75 baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kuufa kwa seli jambo lilochangia kuwa anapoteza kumbukumbu na kukosa utimamu wa akili.

6 – Ni nambari ya jezi anayovaa kiungo fundi wa kudemka na mpira kutoka klabu ya Manchester United, Paul Pogba. Nyota huyo mwenye miaka 28 ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya klabu ya Manchester United kutoa assist nne kwenye mchezo mmoja wakati timu yake ilipocheza dhidi ya Leeds Utd na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1.

Pogba anakuwa mchezaji wa saba kwenye historia ya EPL kutoa assist nne kwenye mchezo mmoja na kuungana na nyota wane wa zamani wa Arsenal, Dennis Bergkamp, Jose Antonio Reyes, Cesc Fabregas, Santi Carzola, Emmanuel Adebayor nyota wa zamani wa Spurs na Harry Kane nahodha wa sasa wa Spurs.

5 – Ni idadi ya miaka ambayo winga kiberenge kutoka timu ya taifa ya Mapharao, Mohammed Salah ameitumikia klabu ya Liverpool almaarufu ‘Majogoo wa jiji’ akitokea klabu ya AS Roma ya nchini Italia mwaka 2017.

Salah ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee tokea kuanzishwa kwa Ligi kuu ya England kufunga bao kwenye kila mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo kwa misimu mitan mfululizo tokea mwaka 2017. 

Salah alianza kuandika rekodi hiyo baada ya kuwafunga Watford bao 1 msimu wa 2017/18, kuwafunga Westham Utd bao 1 msimu wa 2018/19, kuwafunga Norwich bao 1 msimu wa 2019/20, msimu wa mwaka 2020/2021 kuwafunga leeds Utd mabao 3 na msimu huu amewanyuka Norwich bao 1.

4 - Ni idadi ya mapambano aliyoshinda bondia Jordan Weeks raia wa Marekani aliyedundwa wikiendi hii na mjukuu wa Gwiji wa Masumbwi Duniani Muhammed Alli, Nico Ali Walsh.

Nico Ali Wash alitumia sekunde 70 za mzunguko wa kwanza kumdunda Jordan Weeks na kuanza vema kwenye safari yake ya masumbwi kumrithi babu yake kwani Nico hilo lilikuwa ndiyo pambano lake la kwanza rasmi kwenye masumbwi ya uzito wa kati. Baada ya ushindi huo Nico amesema amemzawadia babu yake ushindi huo ikiwa ni ishara ya kumkumbuka zaidi tokea afariki 2016.

3 – Ni idadi ya wachezaji wa kigeni waliothibitishwa kusajiliwa na klabu ya Yanga juma lililopita na kuorodheshwa kwenye safari ya kuelekea nchini Morocco kuweka kambi kujiwinda na michezo ya awali ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika pamoja na maaandalizi ya michezo ya msimu ujao.

Wachezaji hao ni kiungo mbabe Khalid Aucho, winga tereza Ducapel Jesus Moloko na mlinzi wa kulia mwenye kama ya mbwa wa polisi ‘Djumaa Shabani’. 

Msafara wa Yanga uliwasili salama Dubai hapo jana huku ukitarajiwa kuondoka saa mbili asubuhi ya leo Agosti 16, 2021 na kuelekea Morocco kwa kambi ya siku 10 kwenye kituo cha King Mohammed VI Football Complex kilichopo kwenye mji wa Sale nchini humo.

2 - Ni idadi ya awamu alizofanyiwa upasuaji mcheza tenisi anayeshika nafasi ya 9 kwa ubora Duniani kwa upande wa wanaume, Mswiss Rodger Federer katika mwaka 2020 na kumfanya akae nje ya mashindano kwa vipimo tofauti tofauti.

Mkali huyo anayeongoza kuwa na grand slam nyingi, grand slam 20 sawa na Rafael Nadal wa Hispania na Novak Djokovic wa Serbia, Federer ameweka wazi kuwa anataraji kufanyiwa upasuaji wa goti tena ndani ya siku chache jambo ambalo litamuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili jambo lililozua hofu kubwa kwa nyota huyo kuikosa michuano ya tenisi ya US open inayotaraji kufanyika tarehe 30 Agosti 2021.

Ukiondoa Federer kutolewa kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano ya Wemblidon lakini alikosa michuano ya Tokyo Olympic kutokana na hofu ya kupata majeraha hayo ya goti.

1 – Ni idadi ya klabu pekee aliyochezea gwiji wa zamani wa soka nchini Ujerumani, Gerd Muller aliyeitumikia klabu ya Bayern Munich na kuweka historia nyingi za kibabe. Taarifa za kuhuzunisha ni kwamba nyota huyo amefariki Dunia siku ya jana na kuacha vilio tele nchini Ujerumani na Duniani kwa ujumla wake.

Gerd Muller alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye umahiri mkubwa wa kufunga mabao kwa ustadi tena kwa idadi kubwa.

Baadhi ya rekodi za kibabe anazoshikilia nyota huyo, kuwa mfungaji bora mara saba kwenye ligi kuu ya Ujeriumani akifanikiwa kufunga mabao 365 kwenye michezo 427 aliyocheza na kustaafu soka mwaka 1982.

Gerd atakumukwa hasa na wapenzi wa Bayer Munich kwa kusaidia timu hiyo kutwaa matajai mengi ikiwemo Bundesliga 4, DFB mataji matatu na kutwaa kombe la Dunia la mwakak 1974 kwa upande wa timu ya taifa.