Wednesday , 8th Sep , 2021

Klabu ya Yanga SC, kupitia msemaji wao Haji Manara imethibitisha kuwa itawakosa wachezaji wake wakimataifa kuelekea mtanange wa ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Rivers United kwenye hatua ya awali utaofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Djuma Shaban ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kukosa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Rivers United.

Wachezaji hao ni Khalid Aucho wa Uganda, beki Djuma Shaban na mshambualiaji Fiston Mayele wote kutoka DR Congo, watakosa mchezo huo kwasababu ya kukosa hati ya Uhamisho wa kimataifa (ICT).

Manara amesema kuwa kutokana na klabu ya El Makkasa ya Misri kuchelewesha ICT ya Aucho kama ilivyokuwa kwa AS Vita, Yanga wameomba vibali vya wachezaji hao kupitia FIFA,.Kosa kama hilo lilifanyika tena nchini DR Congo ambapo klabu za Union Maniema na AS Vita nazo hazikutuma vibali kuthibitisha uhamisho wa wachezaji Shaban na Mayele.

Ripoti zinasema kuwa Yanga walikuwa na madeni ambayo waliyopaswa kupeleka uthibitisho wa malipo kwa wakati, ingawa Afisa Habari wa Yanga, Haji Manara amekanusha uvumi huo.

Katika hatua nyingine Manara amesema kuwa kuelekea mchezo huo dhidi ya Rivers United siku ya Jumapili, wataelekea uwanjani na kauli mbiu inayosema mabingwa wamerejea ''The return of Champions'', huku akiweka wazi kuwa wanangoja taarifa rasmi kutoka kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF) juu ya idadi ya watazamaji watakaoruhusiwa hudhuria mchezo huo kupitia TFF.

Vilevile Manara ameongeza kuwa, vipaumbele vyao msimu huu ni kutwaa mataji yote ya hapa nchini (TPL,ASFC na Mapinduzi Cup) wakati wakitarajia kuvuka hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa barani Afrika.