Thursday , 23rd Sep , 2021

Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Tanzania bara, Mtibwa Sugar wameweka wazi kuwa malengo yao makubwa msimu ujao ni kuhakikisha wanarejea katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa TPL huku akisisitiza kuwa Yanga, Simba na wao ndio timu bora katika ardhi ya Tanzania.

Afisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobius Kifaru katika moja ya mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita.

Hayo yamesemwa na Afisa Habari wa Wakatamiwa hao, Thobius Kifaru Ligalambwike akiwa anatuthibitishia kuwa aliyekuwa kocha wa vilabu vya Simba na Azam, Joseph Marius Omog ameshajiunga nao tayari kwa kukiandaa kikosi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu.

''Mwali wetu ameshawasili, tulikuwa na barua za maombi takribani 70, lakini tumeamua kumchukua Jospeh Omog ambaye analijua soka la Tanzania vizuri, amefanya Azam na Simba, tunaamini atatufikisha mbali, nawakumbusha timu tatu bora nchini ni Simba, Yanga na Mtibwa, hivyo tunarejea katika nafasi yetu''Alisema Thobius Kifaru.

Kifaru amesema  raia huyo wa Cameroon akichagizwa na usajili maridhawa walioufanya kwa kuwajumuisha mlinzi Abdi Banda,kiungo Said Ndemla kutawapa makali ya kutikisa katika Ligi Kuu Tanzania bara.