Tuesday , 9th Nov , 2021

Baada ya kuonesha kiwango bora kwenye mwezi wa Oktoba, Kiungo wa Yanga Feisal Salum amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi, huku kocha wake Nasreddine Nabi akiteuliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Feisal Salum anachukua tuzo hiyo baada ya kuwashinda Ramadhan Chombo wa Biashara na Fiston Mayele wa Yanga, Huku Kocha Nabi akiibuka kidedea mbele ya Mbwana Makata wa Dodoma Jiji na Francis Baraza wa Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 8, 2021 na Bodi ya Ligi, mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi wa kwanza wa msimu, Septemba huku kocha wake, Malale Hamsini akiteuliwa Kocha Bora mwezi huo wa tisa.

Mayanga anatwa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Obrey Chirwa wa Namungo na Cleophas Mkandala wa Dodoma Jiji, huku Kocha wake Malale Hmasini akiibuka kifua mbele dhidi ya Hemed Suleiman wa Namungo na Hararimana Haruna wa Mbeya Kwanza.

Aidha, Tumaini Ikomba ameteuliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja mwezi Septemba kwa uzuri wa Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu mkoani Arusha na Modestus Mwaluka amekuwa Meneja Bora wa Oktoba kwa kazi yake nzuri katika Uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya.