Friday , 14th Jan , 2022

Wekundu wa Msimbazi Simba wameibuka kuwa mabingwa wa Michuano ya kombe la Mapinduzi mwaka 2022 baada ya usiku wa jana Januari 13, 2022 kuifunga Azam 1-0 kwenye dimba la Amani, Visiwani Zanzibar.

(Wachezaji wa SImba wakisheherekea Ubingwa wa Mapinduzi mwaka 2022)

Bao la pekee la ushindi la SimbaSC limefungwa na mshambuliaji wake, Meddie Kagere dakika 56 kwa mkwaju wa penalty baada ya mlinda mlango wa Azam FC, Mathias Kigonya kumkanya Pape Ousmane Sakho ndani ya eneo la 18.

Ubingwa huo umewafanya Simba kubeba kombe hilo mara ya nne, kufuta uteja mbele ya Azam FC wa kupoteza fainali mbili mbele ya Wanalamba lamba hao pamoja na kujiuliza vema walipopoteza 2021 mbele ya watani wao, Yanga.

Kamati ya mashindano ya Mapinduzi iliwapa zawadi Simba ya Shilingi milioni 25 taslimu kwa kuwa bingwa huku Makamu Bingwa, klabu ya Azam walipewa kiasi cha shilingi milioni kumi na tano taslimu.

Mbali na zawadi za Jumla, lakini kamati hiyo iliendelea kutoa tuzo binafsi kwa wachezaji waliofanya vema ambapo, tuzo ya mfungaji bora imeenda kwa Meddie Kagere, Kipa bora, Aishi Manula na Mchezaji bora Pape Sakho wote wa Simba SC.

Henock Inonga Baka alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo wa fainali hiyo baada ya kuonesha umahiri mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya Azam FC kwa washambuliaji Rodgers Kola na Idris Mbombo.

Tuzo ya mchezaji bora chipukizi imeenda kwa winga Tepsi Evans, kiungo bora imeenda kwa Kenneth Muguna, beki bora Daniel Amoah wote kutoka kikosi cha mabingwa wa Kihistoria wa michuano hiyo, Klabu ya Azam.