(Viungo wa Simba SC, Mzamiru Yassin na Rally Bwalya)
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema nyota hao wawili waliachwa kwenye safari ya mechi za kimataifa walizocheza hivi karibuni ugenini kufuatia kuwa na matatizo ya kifamilia.
"Mzamiru na Bwallya hawakuwa na majeraha bali walipata msiba hivyo tuliamua kuwaacha nchini wakashughulikie matatizo ya kifamilia na mara baada ya kurejea wameungana na wenzao kwenye Uwanja wetu wa mazoezi kujiandaa na mechi dhidi ya Biashara Mara United''
''Kuhusu Hassan Dilunga Kibu Denis na Chris Mugalu tunasubiri ripoti ya tabibu, pia Jonas Mkude tulirejea naye bado afya yake haijaimarika vizuri hivyo ni mapema kusema iwapo atacheza mechi ya ijumaa'' amesema Ahmed Ally.
Vilevile Ahmed Ally amesema mzunguko wa pili ndio muda ambao wanapaswa kushikamana ili wahakikishe wanatwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara kwa msimu wa tano mfululizo.
''Wana Simba tunapaswa kushikamana ili tufanikishe mipango yetu, ni nyakati ngumu, ushindani mkubwa safari hii,lakini tunajua namna ya kuuchukua ubingwa hivyo tumejipanga kufunga hesabu zetu'' amesema Ahmed Ally.
Simba inakutana na Biashara Mara United ambayo katika mechi ya duru la kwanza ilimalizika kwa suluhu. Wekundu wa Msimbazi wanakamata nafasi ya pili wakiwa na alama 31 baada ya mechi 15,wakati Biashara Mara United ipo nafasi ya 14 wakiwa na alama 15 .



