Thursday , 28th Apr , 2022

Mshambulijai wa Chelsea,  Romelu Lukaku atalazimika kupunguza mshahara wake kwa nusu nzima ili kukamilisha ndoto zake za kurejea kukipiga tena katika timu ya Inter Milan Nchini, Italia.

Staa huyo wa Chelsea, Lukaku, 28, amefichua mipango yake ya kurudi kwenye mikikimikiki ya Serie A, Desema mwaka jana baada ya kukipiga Stamford Bridge alikorejea kwa mara ya pili kwa kipindi cha miezi minne tu.

Na kinachoelezwa ni kwamba Lukaku hata amewasiliana kwa simu ya video na bosi kubwa wa Inter Milan akimweleza dhamira yake ya kutaka kurudi Italia.

Na miamba hiyo Nerazzurri imeripotiwa sasa ipo tayari kumrudisha Lukaku na kumtimizia ndoto zake baada ya hapo awali kufuta mpango wa kumsajili tena straika huyo. Lakini, shughuli itabaki kwa Lukaku kama atataka kurudi San Siro.

Mbelgiji huyo kwa sasa analipwa Pauni 325,000 kwa wiki baada ya kukamilisha usajili wake wa Pauni 97.5 milioni huko Stamford Bridge. Lakini, kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ya Inter Milan mshahara wake unaweza kuwa tatizo, hivyo Lukaku atalazimika apunguze walau nusu ya mshahara wake, ili apokee Pauni 5.5 milioni kwa mwaka ili arudi Inter kwa mujibu wa Football Italia.

Hata hivyo, kinachoelezwa ni kwamba pesa si tatizo kwa Lukaku, yupo tayari kufanya hivyo ili kutimiza ndoto zake. Hapo shida inarudi kwa Inter, ambao watalazimika kulipa pesa ndefu kumsajili Lukaku kutokana na kuwa na kusaini miaka mitano Chelsea aliponaswa mwaka jana.

Paris Saint-Germain nayo inaripotiwa kumtaka Lukaku kama Inter itashindwa kumsajili.