Tuesday , 10th May , 2022

Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya Sportpesa imetoa kitita cha shilingi milioni 50 kwa klabu ya Simba kama bonus baada ya kufanikiwa kufika robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mujibu wa mkataba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, amemkabidhi Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez, hundi ya Shilingi milioni 50

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Sportpesa, Tarimba Abbas ameipongeza Simba kwa mafanikio waliyopata kwa miaka minne katika mashindano ya kimataifa na ligi za ndani.

"Hii ni mara ya nne kuwakaribisha Simba katika ofisi zetu kwa shughuli kama hii. Katika mkataba wetu kuna makabaliano ambayo wanapofikia hatua fulani kuna bonus wanapata na leo tumekamilisha. Sio siri Simba imeutendea haki mkataba huu na wametutungaza vizuri," amesema Tarimba.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba, Barbar Gonzalez ameishukuru Sportpesa kwa kufuata makubaliano ya mkataba na amekiri kuwa anaamini baada ya mazungumzo kukamilika tutasaini mkataba mpya.

"Kwa niaba ya klabu ya Simba tunawashukuru Sportpesa kwa kufuata makubaliano ya mkataba kwa kutoa bonus hii ya Sh. 50,000,000 sisi tunawaahidi tutaendelea kufanya vizuri na kuchukua tena na tena bonus hizi," amesema Barbar.