Monday , 13th Jun , 2022

Ligi Kuu soka Tanzania bara NBC Premier League inarejea tena leo kwa kuchezwa michezo miwili. Ligi inarejea tena baada ya kusimama kwa takribani wiki mbili kupisha kalenda ya kimataifa ya FIFA, michezo hii inayoanza kuchezwa leo ni ya raundi ya 27.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zilitoka sare ya bao 1-1

Mchezo wa mapema leo unachezwa saa 8:00 mchana ambapo klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting ya Pwani, mchezo huu unachezwa uwanja wa Manungu huko Turiani Morogoro.

Timu hizi zote zina alama sawa 28 katika michezo 26, kwenye msimamo wa Ligi Mtibwa wapo nafasi ya 12 juu ya Ruvu shooting walionafasi ya 13. Mtibwa wamekaa juu ya Ruvu kwa faida ya tofauti ya magoli machache ya kufungwa.

Mchezo wa pili unachezwa Saa 10:00 jioni mkoani Geita Uwanja wa Nyankumbu wenye wa Mchezo ni Geita Gold FC watacheza dhidi ya Dodoma jiji Fc. Mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizi zilitoka sare ya bao 1-1 mchezo ambao ulikuwa wa kwanza timu hizi kukutana kwenye Ligi Kuu.

Geita wapo nafasi ya 5 kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na alama 36 na wameizidi Dodoma Jiji alama 5, Dodoma wapo nafasi ya 11 wakiwa na alama 31.