Friday , 22nd Jul , 2022

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limewakamata watu tisa wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kuwajeruhi baadhi yao baada ya kuwakuta wakishiriki tukio la ujambazi usiku wa kuamkia leo Julai 22, 2022, maeneo ya kiwanda cha Sheri Automotive Germany kilichopo Keko wilayani Temeke. 

Baadhi ya silaha walizokuwa nazo majambazi hao

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo Jumanne Muliro, na kusema watuhumiwa hao wa ujambazi walijihami kwa silaha na kuanza kuwashambulia askari kwa risasi na ndipo walipodhibitiwa.

Kamanda Muliro amesema baada ya kupekuliwa watuhumiwa hao, walikutwa na bastola moja iliyofutwa namba, silaha za jadi mapanga manne na funguo nyingi aina mbalimbali za kufungulia magodown na ofisi za kiwanda hicho, gari No. T 201 DXN HIACE ikiwa tayari imemekwisha pakiwa mali za wizi box zaidi ya 70 za vipuri.