Thursday , 29th Sep , 2022

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) siku ya leo wamechangia taulo za kike pakiti 1500 katika kampeni ya Namthamini ambazo zitaweza kuwasaidia wanafunzi 125 kwa mwaka mzima wakiwa shule.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye akikabidhi taulo za kike kwa Meneja Mahusiano wa IPP, Nancy Mwanyika.

TEA wamekabidhi taulo za kike katika ofisi za East Africa TV na East Africa Radio ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye amesema wametoa mchango wao ili kuwasaidia wanafunzi wanaosoma katika mazingira magumu wasikose masomo yao shuleni wakiwa katika kipindi cha hedhi.

Kampeni ya Namthamini imejikita katika kuwasadia wanafunzi wa kike mashuleni kupata taulo za kike na kuhakikisha elimu ya hedhi salama inafika kwa wanafunzi nchini.

Pia Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye alipata nafasi ya kuongea katika kipindi cha MamaMia cha East Africa Radio na kipindi cha DADAZ cha East Africa TV na kueleza namna walivyoguswa na kuamua kuchangia kampeni ya Namthamini.

Kampeni ya Namthamini ilizinduliwa Mei 27 mwaka huu, na Septemba 19 mwaka huu ilianza kugawa taulo za kike mashuleni kwa kuanzia katika mkoa wa Mtwara, ambapo shule 9 kutoka Wilaya ya Mtwara, Masasi na Nanyumbu zilipatiwa taulo za kike jumla ya pakiti 6,937 kwa wilaya zote tatu.