Tuesday , 25th Oct , 2022

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Rashid Mchatta amewataka watumishi wa umma kutumika mifumo rasmi ya uendeshaji shughuli za serikali ikiwemo mabaraza ya wafanyakazi kuongeza tija mahala pa kazi.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Rashid Mchatta

Akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo Oktoba 25, 2022 mjini Sumbawanga, Mchatta amesema ni wajibu wao kuzingatia taratibu za utumishi wa umma.

“Tutumie mifumo rasmi ikiwemo mabaraza ya wafanyakazi kutoa mchango wa kuboresha utendaji kazi wa serikali. Kila mmoja wenu anapaswa kujua dira na mwelekeo wa taasisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”alisisitiza Mchatta.

Katika kikao hicho, Mchatta amewataka watumishi hao kuelewa dira ya mkoa huo ili wachangie kuleta maendeleo kwa ustawi wa wananchi ambapo amesisitiza pia kudumisha nidhamu mahala pa kazi.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mchatta ametoa wito kwa wakuu wa idara na vitengo pamoja na Makatibu Tawala Wilaya kuendelea kufanya usimamizi wa karibu na kuhakikisha ifikapo Mwisho wa mwaka huu wa fedha ziwe zimetumika kwa mujibu wa sheria.