Sunday , 30th Oct , 2022

Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imetangaza kuwepo kwa nafasi  ya Ubunge katika jimbo la Amani , Tanzania Zanzibar kutokana na kutokea kifo cha  aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mussa Hassan (CCM) kilichotokea Oktoba 13, 2022, pamoja na nafasi za madiwani katika kata 12 Tanzania Bara.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 30 na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dk. Wilson Charles ambapo amesema, Tume imepokea barua kutoa kwa Spika wa bunge la Tanzania na barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania bara ikitaarifu kuwepo kwa nafasi hizo. 

Aidha anesema kuwa ratiba ya uchaguzi mdogo itaanza Novemba 24 hadi 30 ,2022 ambapo kutakuwa na zoezi la kutoa fomu, Novemba 30, 2022 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea, Desemba 01 hadi Desemba 16, 2022 itakuwa kampeni za uchaguzi, Desemba 17, 2022 itakuwa siku ya kupiga kura.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevikumbusha vyama vya siasa pamoja na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi, taratibu miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume katika kipindi chote cha uchaguzi mdogo.