Wednesday , 2nd Nov , 2022

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera inawashikilia mawakala watano wa kampuni za simu za mkononi ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, kwa tuhuma za kuwasajilia watu namba za laini za simu kwa kutumia majina na vitambulisho vya watu wengine

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Kagera John Joseph

Mkuu wa TAKUKURU  mkoani Kagera John Joseph amesema kuwa watu hao walibainika katika uchunguzi wa taasisi hiyo uliofanyika katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, na kwamba baadhi ya laini hizo hutumika katika uhalifu.

"Kwa sababu tumebaini kuna baadhi ya namba zimesajiliwa kwa kutumia majina ya watu wengine, na ukifuatilia unakuta ni mtu mzima na wengine ni marehemu, lakini laini hizi zipo zinaendelea kufanya kazi, kwa hiyo niwaombe wana Kagera waende kwa mawakala wa simu na kuangalia namba zao za NIDA zimesajili namba ngapi za simu, ukikuta kuna namba huzifahamu wataarifu watu wa mitandao ya simu wakazifute kwa sababu zinaweza kutumika kufanya uhalifu" amesema John Joseph 

Wakizungumzia suala hilo baadhi ya wakazi wa manispaa ya Bukoba wameomba serikali kuwachukulia hatua kali mawakala watakaobainika kuhusika na tatizo hilo, ili kuwaepusha na madhara yanayoweza kuwakumba ikiwamo kuhusishwa na uhalifu hasa wa mtandaoni

"Hii ni changamoto ambayo TCRA wanapaswa kuishughulikia, mwananchi ambaye kitambulisho chake kinatumika kusajilia watu wengine yeye hafahamu chochote, na masuala ya utapeli yanapitia huko huko mtu unatumiwa meseji tano hadi kumi wakikutaka utume pesa, hili liko ndani ya serikali kama italivalia njuga kupambana nalo, litakwisha" amesema.