Wednesday , 2nd Nov , 2022

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta binafsi ihakikishe inakamilisha taratibu za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji mto Rufiji utakaosambaza maji katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Tanzania Kassim Majaliwa

Aidha Waziri Mkuu ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) iendelee kutenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima zaidi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji. 

Majaliwa ametoa maagizo haya leo Jumanne, Novemba 2, 2022 baada ya kukutana na Waziri wa Maji, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wa DAWASA kwa ajili ya kujadili hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu amesema serikali itahakikisha maeneo yote yanapata huduma za maji na kazi ya uchimbaji visima pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji inaendelea ili kufikia matamanio ya Rais Samia ya kufikisha huduma ya maji karibu na makazi ya wananchi.