Friday , 4th Nov , 2022

Wafanyabiashara wa soko la wakulima la Nyankumbu Halmashauri ya mji Geita, wameugomea uongozi wa Halmashauri hiyo uliowataka kuhama ndani ya siku tatu kwenye soko hilo na kwenda soko la Mbagala ambalo wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilikimbia kutokana na kutokuwa na wateja.

Mmoja wa wafanyabiashara akiangua kilio

Wakizungumza na EATV mamia ya wafanyabiashara kwenye soko hilo wameuomba uongozi kuwataji vitu wanavyovitaka ili waendelee kuwepo kwenye soko hilo.

Katibu wa soko hilo Daniel Lukumbisi, amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo aweze kufika eneo la soko hilo aongee na wafanyabiashara ili waweze kumaliza mgogoro huo ambao wafanyabiashara hawapo tayari kuhama kwenye soko hilo rasmi.

"Zoezi hili mimi naona halijakaa vizuri kwa sabau watu wana mikopo yao, wangeacha wafanyabiashara ili waendelee na biashara zao na maisha mengine yaendelee, mimi nafikiri Mkurugenzi afike hapa aongee na wafanyabiashara, nini kinatakiwa kifanyike basi, akifika hapa wafanyabiashara wakaongea kero zao nafikiri watamuelewa," amesema Lukumbisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Zahra Michuzi, na Mkuu wa wilaya hiyo Wilson Shimo, wamezitaja sababu za kuwataka wafanyabiashra waweze kuhama kwenye soko hilo ni uwepo wa msongamano mkubwawa watu na bidhaa na hivyo kutaka wawatawanye kwenye masoko mengineyo.