Thursday , 10th Nov , 2022

Mkuu wa mkoa  wa Mwanza Adam Malima ameiagiza  mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira MWAUWASA kumpelekea ripoti kwanini ujenzi chanzo cha maji kilichowekwa jiwe la msingi na makamu wa Rais Dkt Phillip Mpango umeshindwa kukamilika kwa wakati

Mnamo mwezi September mwaka huu Makamu wa Rais Dkt Mpango akiwa kwenye ziara jijini Mwanza aliagiza chanzo hicho cha maji kikamilike mwishoni mwa mwezi ujao, na hapa mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima akaagiza MWAUWASA kuandika ripoti ya ujenzi huo kutokamilika kwa wakati

‘Kwahiyo wametupa mwezi wa sita maelekezo yangu kwao ni kwamba waende wakaangalie yale yaliyosemwa wakati makamu wa Rais yupo hapa na yanayosemwa leo na namna yanavyoweza kufanyiwa uboreshaji kisha taarifa hiyo wanipe nakala moja mimi lakini mwenye taarifa yake ni Waziri wa maji Jumaa Aweso aweze akiipata atajua namna ya kumfikishia makamu wa Rais na utekelezaji uendelee wakati marekebisho yanafanyika’

Kwa upande wake mhandisi mshauri wa mradi huo Olivier Viguier amesema mradi huo utakamilika mwezi wa sita mwakani kufuatia vifaa vingi vya ujenzi huo kutoka nje ya nchi

‘Kwa jinsi tulivyokuwa tumepanga kumaliza mradi huu mwezi wa pili naona itashindikana kutokana na vifaa vingi kuwa havitengenezwi Tanzania vinaagizwa nje ya nchi kwa hiyo baadhi ya kazi hazitakamilika hadi tusubiri vifaa na mitambo kutoka nje ya nchi hivyo kazi inaweza kufika hadi mwezi wa sita mwakani’

Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mwanza MWAUWASA Leonard Msenyele amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea  vizuri ambapo kipindi makamu wa Rais anaweka jiwe la msingi ulikuwa umefikia asilimia 43 na kwa sasa umefikia asilimia 54

"Tutaiandaa taarifa ambayo mkuu wa mkoa ameelekeza tuifanyie kazi na hatimaye tuitoe kwa hali halishi ya utekelezaji wa mradi kwa maelekezo ya makamu wa Rais alitoa maekezo tutafanya hiyo kazi na kuhakikisha mradi huu unakamilika"

Kukamilika kwa chanzo hicho cha maji kitakachogharimu Zaidi ya shilingi bilioni 69kunatarajiwa kupunguza changamoto ya ukosefu wa maji kwa wakazi wa jiji la Mwanza ambapo mahitaji kwa siku ni lita milioni 160 kwa sasa lita milioni 90 pekee ndiyo zinapatikana huku lita milioni 30 hupotea.