Friday , 9th Dec , 2022

Hatma ya Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi na wafuasi wake nane kufungwa gerezani au kuachiwa huru katika kesi ya jinai namba 10/2022 itajulikana Desemba 22 mwaka huu baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake.

Katika kesi hiyo namba 10 ambayo mfalme Zumaridi na wafuasi wake wanashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kufanya shambulio la kudhuru mwili, upande wa utetezi umefunga ushahidi wake na mashahidi 10 huku vielelezo 11 vikitolewa na upande wa mashtaka

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekobora amesema kesi hiyo itaendelea Desemba 22 mwaka huu Saa tatu asubuhi kwa ajili ya usomaji wa hukumu hiyo

Kabla hakimu anayesikiliza kesi hiyo hajataja tarehe ya hukumu, upande wa utetezi ulihitimisha ushahidi wake kwa mashahidi wawili kutoa ushahidi wao ambao ni mshtakiwa namba moja Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi na mshtakiwa mwingine aitwaye Suzan Simon

Akianza kutoa ushahidi wake shahidi wa utetezi, Suzan Simon (29) aliieleza mahakama hiyo kuwa alilazimika kwenda kwa Zumaridi baada ya kutelekezwa na mzazi mwenzake, Ally Abbas.

Ameieleza mahakama kuwa pamoja na kuishi na Abbas kwa miaka mitano kabla upendo wao haujakoma, walipeana talaka ndipo mgogoro wa kugombea mtoto ulipoibuka na kusababisha mwanaume amfungulie kesi ya kudai mtoto  katika Mahakama ya mwanzo Mkuyuni jijini Mwanza.

Akasema mahakama ya mwanzo Mkuyuni ilitoa hukumu kuwa ampe mtoto mzazi mwenzake  lakini hakuridhishwa na uamuzi huo ndipo akakata rufaa mahakama ya wilaya, kabla hukumu yake haijatolewa akashangaa anakamtwa na kupelekwa rumande na kuamriwa avue viatu na kunyang'anywa  simu kisha kuungwanishwa na washtakiwa wengine na kupewa kesi

Kwa upande wake, shahidi wa mwisho wa utetezi katika kesi hiyo, Mfalme Zumaridi ameieleza Mahakama hiyo kwamba wakati wa ukamataji askari polisi walichukua Sh19.5 milioni chumbani kwake pamoja na kadi yake ya Chama cha Mapinduzi, hati tano za nyumba, kadi mbili za benki (Equity na CRDB), simu mbili aina ya Samsung na Infinix.

Akaongeza kuwa askari hao wakiongozwa na Inspekta Mapunda pia walichukua kadi ya gari aina ya Harrier na Toyota Wish, hati ya kusafiria, kitambulisho cha Nida, cheti cha kuzaliwa na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake, David Moses na Edward Moses.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi, Erick Mutta, Zumaridi alisema askari hao walipoingia ndani ya uzio wa geti la nyumba yake walipiga mabomu ya machozi huku wakishambulia watu waliokuwemo ndani wakiwemo mafundi ujenzi kwa kutumia virungu, nyaya za umeme na vitako vya bunduki.

Aidha Zumaridi ameiambia mahakama kuwa askari hao Walivyoingia chumbani kwake walimpiga sana huku askari mmoja akimtaka aonyeshe pesa zilipo akawa amenyamaza tu ndipo wakaanza kumvuta wakamtoa nje ya chumba chake  na kumwambia alale chali aangalie  jua kisha askari hao wakarud chumbani kwake na kuchukua fedha na vitu vingine 

Baada ya maelezo hayo, Hakimu, Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 22, mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kutoa hukumu ya kesi hiyo.