Thursday , 29th Dec , 2022

Wakazi mkoani Kagera hasa katika Manispaa ya Bukoba wametakiwa kutoa maeneo yao bila kudai fidia ili kuruhusu Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kupitisha nguzo za umeme, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma hiyo kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000. 

Wananchi wa Manispaa ya Bukoba

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo katika Kata ya Ijuganyondo iliyoko katika manispaa ya Bukoba, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, amesema kuwa miradi yote iliyoko chini ya REA haina utaratibu wa kulipa fidia, na kwamba wanaotekeleza mradi huo wanafahamu kuwa kuna mazao ya wananchi katika mashamba hivyo watatumia busara wakati wa utekelezaji. 

"Nimeamua kulisema hili hapa kwa sababu ni mradi wa kwanza wa aina hii kwenu huko vijijini wanalijua hili, niwaombe viongozi wakiwamo wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani na vyama vya siasa wa maeneo ambayo mradi huu utapita, kukaa vikao na wananchi na kufanya mikutano ya haraka, ili kukubaliana na mkandarasi wapi wapitishe laini za umeme" amesema Byabato

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA Tanzania Mhandisi Hassan Said, amesema kuwa wao pamoja na kwamba jukumu lao ni kupeleka umeme vijijini, lakini walifikia uamuzi wa kuwahudumia pia wananchi wanaoishi pembezoni mwa miji, manispaa na majiji, kutokana na maeneo hayo kuwa na watu ambao maisha yao hayana tofauti na wanaoishi vijijini.